Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa ufafanuzi juu ya kauli aliyotoa Spika wa Bunge jana asubuhi bungeni kuhusu malipo ya ndege ambayo ilitumika kumsafirisha Mbunge Tundu Lissu kwenda Nairobi kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Bunge imesema kuwa watu wanaosema Spika wa Bunge amedanganya bunge si sahihi kwani wao wanadai Job Ndugai alieleza kuwa taratibu zote za ndege iliyomsafirisha Tundu Lissu iliratibiwa na Mbunge wa Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky na bunge kusaidia.
Naye Mbunge wa Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky alisema jana kuwa CHADEMA ndiyo imelipa gharama za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Kenya na kuongeza kuwa yeye aliwadhamini wakati huo kwa kuwa hawakuwa na fedha taslimu za kulipa.
“Mimi nilitumia uwezo niliojaliwa na Mungu nikatafuta ndege kwa ‘flight link’ ambao ni ndugu zetu tunafanya nao biashara sana wakakubali kutusaidia kwa dolla 9,200, ile ndege mimi ndiyo niliita kwa kukubaliana na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kwamba nisimamie mambo hayo baadaye wao waje kurejesha na ndicho kilichotokezea” alisema Turky
Taarifa hiyo inafuatia kuwepo kwa Taarifa kuwa Mbunge huyo ndiye aliyelipia gharama za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Kenya kwa matibabu taarifa ambayo imetolewa na Spika wa Bunge jambo ambalo CHADEMA wamelipinga na kusema Spika anapotosha umma juu ya jambo hilo.
Kwa upande wake Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa amesema kuwa fedha hizo za ndege iliyombeba Tundu Lissu kwenda Nairobi nchini Kenya imelipwa na Watanzania ambao walikuwa wanachangia fedha za matibabu kwa Lissu pamoja na CHADEMA wenyewe na si mbunge wa CCM.
0 Comments
Comments
[download bo chart app bit.ly/pakuabochartapp}